Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Hassan Mousawi Safawi, Rais wa Jumuiya ya Kishia ya Jammu na Kashmir, amelaani vikali kitendo cha Donald Trump kumtishia Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Katika ujumbe huo amesema kuwa:
Miaka 1400 iliyopita, Yazid alimtaka Imam Hussein (as) ampe kiapo cha utii, lakini Imam alikataa kutoa utii kwa mtu fasiki na muovu kama Yazid, na kwa kufanya hivyo aliweka wazi mipaka ya haki na batili.
Yazid wa zama hizi – yaani Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel – sasa unataka utii kutoka kwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, lakini kama vile Imam Hussein (as), Imam Khamenei hawezi katu kujisalimisha kwao.
Leo hii, karibu dunia nzima imenyenyekea kwa namna moja au nyingine mbele ya Marekani, lakini nchi pekee inayosimama imara bila kusalimu amri ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, chini ya uongozi wa Imam Sayyid Ali Khamenei.
Sayyid Hassan Mousawi ameongeza kusema kuwa: Tunalaani vikali vitisho vinavyotolewa na Rais wa Marekani na Israel dhidi ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi. Hili ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa dunia nzima.
Ayatollah al-Udhma Sayyid Ali Khamenei ni kiongozi na marjaa wa wafuasi milioni 240 wa Kishia duniani; kwa hivyo, kumtishia yeye ni shambulio la moja kwa moja dhidi ya Uislamu na ulimwengu wa Kishia.
Natoa wito kwa viongozi wa nchi za Kiislamu, mashirika ya haki za binadamu ya kimataifa, na watu wote wapendao amani duniani, kulaani vitisho hivyo vya kiburi na vichocheo vya chuki.
Kuwalenga na kuwatisha viongozi wa kidini ni hatari kubwa kwa amani na utulivu wa dunia.
Mwisho wa ujumbe huo, Sayyid Hassan Mousawi ametoa wito kwa Waislamu wote duniani kuwa katika majlisi, mikutano ya Ijumaa, na katika ibada zao za kijamii na binafsi, wasali kwa ajili ya kumuombea afya na usalama Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi, na kuiombea ushindi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Maoni yako